Ili kuhakikisha wanafunzi wanamaliza mzunguko wao wa shule kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne, kikao cha kutathmini usalama shuleni kimefanyika leo tarehe 28 Mei, 2025 katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kikiwa na lengo la kujadili njia sahihi za kumuepusha mwanafunzi na masaibu yatakayokwamisha kumaliza shule.
Mradi wa Mpango wa Shule Salama unaoratibiwa na Wizara ya OR-TAMISEMI chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la UNESCO umetekelezwa katika shule 10 ndani ya Wilaya ya Chamwino kwa kutoa mafunzo kwa walimu juu ya namna ya kupambana na changamoto mbalimbali zinazochangia mwanafunzi kutomaliza mzunguko wake wa elimu zikiwemo ukatili, utoro na kukosekana kwa chakula shuleni.
Akizungumza wakati akifungua kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji Ndg. Tito Mganwa amewapongeza Walimu kwa jitihada mbalimbali wanazozifanya kuhakikisha wanafunzi wanakuwa salama katika maeneo ya shuleni.
“Ninapenda kuwapongeza kwa jitihada mbalimbali ambazo mmekuwa mkizifanya kuhakikisha kwamba watoto wetu wakiwa shuleni wapo katika mazingira salama, na katika hili kumekuwa na ushirikiano wa kila mmoja lakini bado jitihada nyingi zinatakiwa”. Alisema Ndg. Mganwa.
Kwa upande wake Mratibu wa Mpango wa Shule Salama (SSP-COO) kutoka Wizara ya OR-TAMISEMI Dkt. Theresia Kuiwite amesema lengo kubwa la mradi huo ni kumsaidia mwanafunzi kumaliza mzunguko wake wa masomo kuanzia shule ya msingi hadi sekondari.
“Malengo ya mradi au mpango wa shule salama ni kuhakikisha wanafunzi wanapoanza shule wanamaliza mzunguko wao wa elimu na kwa sasa sera ya elimu wanatakiwa waende mpaka kidato cha nne, kwahiyo ni kazi na jukumu letu kubwa kuhakikisha wanafunzi hawa wanafika kule”. Alisema Dkt. Kuiwite.
Aidha, kuundwa kwa klabu za shule salama shuleni, kuwekwa kwa mabango ya kupinga ukatili maeneo ya shule, wanafunzi kutoa maoni katika sanduku la maoni shuleni pamoja na upatikanaji wa chakula ni miongoni mwa mikakati iliyowekwa katika shule ili kumuwekea mazingira salama mwanafunzi aweze kuhitimu masomo yake kwa ufanisi.
Je, tuambie wewe na jamii yako unazingatia usalama wa mtoto akiwa shuleni?
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.