Katika kufikia azma ya Serikali ya awamu ya sita ya utekeleji wa ajenda ya kilimo ambayo inataka sekta ya kilimo kuchangia Pato la Taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, Halmashauri ya wilaya ya Chamwino imeanza kutekeleza agenda hiyo kwa kuwahimiza wakulima kulima mazao mbalimbali ya umwagiliaji sambamba na ufugaji wa samaki ili kuifanya sekta ya hiyo kuwa ya biashara katika skimu ya umwagiliaji.
Bw.Godfrey Mnyamale ambaye ni mkuu wa idara ya kilimo,umwagiliaji na ushirika kutoka Halmashauri ya wilaya ya chamwino amesema hayo katika viwanja vya nane nane vilivyopo Nzuguni jijini Dodoma ikiwa ni siku chache tangu kumalizika kwa maonesho hayo Augost 10 mwaka 2022.
Akitolea ufafanuzi kuhusu kilimo cha umwagiliani jinsi ambavyo kinaweza kuleta tija kwa wakulima Bw.Mnyamale, anaeleza mikakati mbalimbali ambayo Halmashauri hiyo inafanya katika sekta ya kilimo kwa kushirikiana na wadau wa makampuni ya pembejeo ili kuleta manufaa kwa Watanzania na kuliongezea pato Taifa.
Bw.Mnyamale anesema kuwa katika Halmashauri ya wilaya ya Chamwino wameamua kushirikiana na wadau wa pembejeo pamoja na wakulima kwa ajili ya kujikita zaidi katika maeneo ya umwagiliaji ili waweze kulima mazao ya kutosha na kuuza mahindi mabichi ambayo yanafaida kubwa kuliko mahindi makavu.
"Tunapenda kuishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia vitendea kazi na tumeshajipanga kwa kila afisa ugani kuhakikisha anahudumia wakulima wake ipasavyo kwa ajili ya kufikia malengo ya ajenda ya 2030 ambayo tunayaweka kama Taifa" amesema hayo Bw.Mnyamale.
Mbali na hayo Bw.Mnyamale amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino imeazimia kufikisha teknlojia ya kisasa katika kilimo na ufugaji mpaka vijijini ili wakulima waweze kunufaika na kilimo pamoja na mifugo. Naye mdau wa kilimo kutoka Halmashauri ya wilaya ya Chamwino Bw.Onesmo Poteza ambaye ni bwana shamba wa mbegu za SEED-CO amewataka wakulima wote kulima kilicho cha kisasa ili kupata mazao bora kwa kutumia mbegu za kisasa.
"Sisi kama wadau wa Halmashauri wa wilaya ya Chamwino tunaipongeza Halmashauri hiyo kwa kutupatia nafasi ya kuonyesha mbegu zetu katika maonesho haya ili wakulima waweze kuiona.
" Bw.Poteza mdau wa kilimo amesema kuwa Kuna mbegu ya tumbili 419 ambayo ni mbegu bora inayohimili magonjwa na ukame ambayo tayari imeshaingia dukani.
Kwa upande wake mdau wa Kilimo kutoka Halmshauri ya Chamwino ambaye anajihusisha na uzalishaji wa mbegu za mazao mbalimbali kutoka kampuni ya SEED OVER SEED amewataka Watanzania kutumia mbegu ambazo ni bora katika kilimo. Akizungumzia mbegu ambazo zinazalishwa na kampuni ya SEED OVER SEED ameeleza mbegu zinazopatika katika kampuni hiyo ikiwemo mbegu ya kabichi ambayo inaweza kukomaa kwa siku 75 na kufikia uzito wa kilo 6 hadi kilo 10 pamoja na mbegu ya pilipili hoho, maharage lishe ambayo yana madini ya Iron na madini ya zink.Amesema ni mbegu bora ambazo zinauwezo wa kumfanya mkulima akalima na kuvuna kwa haraka bila kupata hasara kwani mbegu hizo ni himilivu.
"Tuna maharage lishe ambayo yameongezewa virutubisho vya aina mbalimbali ikiwemo madini ya Iron pamoja na Zink ambayo yanaimarisha mifupa pamoja na macho ambayo yaliletwa kwa ajili ya kuepusha ulemavu kwa watanzania nchi nzima"
Maonesho ya siku kuu ya wakulima nane nane mkoani Dodoma yalifanyika katika viwanja vya Nzuguni Jijijni hapa ambayo yalifunguliwa na kuhitimishwa na mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, ambapo katika maonesho hayo Halmashauri ya wilaya ya Chamwino imefanikiwa kupata mshindi wa kwanza katika kundi la wakulima bora wa kilimo cha kutegemea mvua Bw.ALISENI DAMIANI ambaye alipatiwa hati ya ushindi huku pia Halmashauri ya wilaya ya Chamwino ikipatiwa hati ya mshindi wa tatu katika kundi la Halmashauri za mkoa wa Dodoma.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.