Kuelekea maadhimisho ya miaka 63 ya uhuru wa Tanzania Bara, Wilaya ya Chamwino imefanya mdahalo kuenzi uhuru huo wa miaka 63 wa Tanzania Bara uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa shule ya sekondari Chamwino.
Mdahalo huo uliongozwa mbele ya mgeni rasmi Katibu Tawala wa Wilaya ya Chamwino Bi. Neema Nyalege ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mh. Janeth Mayanja katika kuadhimisha miaka 63 ya uhuru wa Tanzania Bara uliopatikana mnamo mwaka 1961 na kilele cha maadhimisho hayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 9 Desemba.
Pia kuelekea katika maadhimisho hayo ambayo kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo “Uongozi Madhubuti na Ushirikishwaji wa Wananchi ni Msingi wa Maendeleo Yetu” yalipambwa kwa mdahalo huo ambao ulibeba mada kuu mbili zilizochangiwa na washiriki mbalimbali ambazo ni “Msingi wa Uhuru Wetu na Maendeleo Endelevu ya Taifa Letu” pamona na “Falsafa ya 4R, Uongozi Madhubuti na Ushirikishwaji wa Wananchi katika Ujenzi wa Taifa Letu”.
Akizungumza katika mdahalo huo Bi. Nyalege amewashukuru washiriki wote walioshiriki katika mdahalo huo kwa kutenga muda wao kuhudhuria mdahalo hasa wanafunzi wa shule za sekondari na msingi kwani wamejifunza mengi kupitia yale yaliyojadiliwa.
Baadhi ya wachangiaji waliochangia mdahalo huo akiwemo Meneja wa Wakala wa Misitu (TFS) Wilaya ya Chamwino Ndg. Samwel Matula ametaja baadhi ya mafanikio yalitokea katika miaka 63 ya uhuru wa Tanzania bara yakiwemo kuanzishwa kwa chuo cha misitu mwaka 1984 Mkoani Morogoro (SUA), pamoja na kuongezeka kwa watumishi katika ngazi ya kila wilaya ambao wanasimamia na kulinda rasilimali za misitu.
Aidha, kwa upande wa Ndg. Godfrey Mnyamale ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Ndg Tito P. Mganwa amepongeza Serikali za awamu zote zilizohudumu baada ya kupatikana uhuru wa Tanzania Bara pamoja na kutaja mafanikio na kupongeza Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya kilimo kwa ongezeko la bajeti ya Wizara ya Kilimo ambapo awali ilipatiwa Tsh milioni 200 tu na kwa sasa imefikia Tsh Trilioni 1.1 ambapo ni ongezeko la zaidi ya asilimia 700 ya bajeti.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.