Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Chamwino Ndugu Athuman H Masasi, amewaapa mwezi mmoja watendaji kata wa halmashauri ya chamwino kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ya halmashauri ili kufikia malengo waliojiwekea kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Ametoa maelekezo hayo jana tarehe 6 Januari, 2021 kwenye kikao kazi kilichowajumuisha watendaji wote wa kata 36 zilizopo katika Halmashauri ya wilaya ya Chamwino kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Ndugu Masasi ametoa mwezi mmoja wa Januari 2021 wa kuwapima, na kufikia mwezi Februari,2021 anataka aone matokeo mazuri kwenye ukusanyaji wa mapato yamepatikana.
‘’Natoa mwezi mmoja wa Januari,2021 na kufikia mwezi Februari nataka nione matokeo mazuri ukusanyaji wa mapato yamepatikana,’’alisema Mkurugenzi Masasi.
Ameelekeza pia wahakikishe kamati za mapato za Kata zilizoundwa ambazo wao ndio wenyeviti zinakutana na kufanya vikao walau mara mbili kwa wiki na kuwasilisha benki mapato yaliyokusanywa kwa kila wiki.
Kwa Watendaji wa Kata ambao jiografia za Kata zao hazijakaavizuri ametoa maelekezo kwa Afisa Utumishi kuhakikisha wanaangalia namna ya kuwapatia usafiri wa pikipiki kwa kuzifanyia matengenezo pikipiki zilizorudishwa na watumishi ambazo hazihitaji matengenezo makubwa.
‘’Afisa utumishi angalia namna ya kuzitengeneza Pikipiki zilizorudishwa na watumishi ambazo hazihitaji matengenezo makubwa na kuwapatia Watendaji waliopo kwenye maeneo yenye mazingira magumu,’’ alisema Mkurugenzi Masasi.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji amewataka Watendaji wa Kata kuhakikisha wanakaa kwenye vituo vyao vya kazi kwani kuna watendaji wengine hawakai vituoni na kwa kufanya hivyo hawawezi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Ameeleza kuwa kuanzia sasa hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya watakaoshindwa kukaa vituoni.
Kuhusu changamoto ya uchache wa mashine za kukusanyia mapato (PoS) Mkurugenzi Mtendaji ameahidi kushughulikia ambapo atahakikisha ameongeza mashine nyingine walau Thelethini (30)kwa maeneo ambayo hayana mashine hizo.
Vilevile katika kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji amemuagiza Kaimu Mweka Hazina wa Wilaya Ndugu Musa Luhamu kuhakikisha anashughulikia changamoto zote za ukusanyaji wa mapato zilizowasilishwa na watendaji hao.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.