Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (Rufaa) Mhe. Jacobs Mwambegele leo Septemba 25, 2025 ametembelea ghala la kuhifadhia vifaa vya uchaguzi na kuangalia vifaa ambavyo vimepokelewa hadi sasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino yenye majimbo mawili ya uchaguzi ya Chamwino na Mvumi.
Mhe. Jacobs Mwambegele amefanya ziara hiyo ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea maeneo mbalimbali nchini kuangalia maandalizi ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza wakati alipotembelea Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino na kupokea ripoti ya utekelezaji wa shughuli za uchaguzi kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Majimbo ya Chamwino na Mvumi Bi. Prudence Kaaya, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele ameagiza watendaji wa uchaguzi kuwa na uadilifu wakati wa utendaji wa majukumu yao.
Halikadhalika amewaasa watendaji hao kuzingatia miiko na miongozo ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ili kuwa na uchaguzi wa haki na usawa
Aidha, amepongeza mwenendo wa mchakato wa uchaguzi unaoendelea hadi sasa nchi nzima pamoja na kuridhishwa na hali ya uhifadhi wa vifaa vya uchaguzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.