Katika mapambano ya kuongeza ufaulu na elimu bora kwa wanafunzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino leo tarehe 30 Januari, 2025 Waheshimiwa Madiwani kupitia Mkutano wa Baraza la Madiwani wa robo ya pili ya mwaka 2024-2025 wameridhia kuanzishwa kwa mfuko wa elimu Chamwino.
Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ukiongozwa na Mwenyekiti Mhe. Edson Sweti ulipitisha ajenda hiyo iliyowasilishwa na katibu wa Baraza hilo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndg. Tito P. Mganwa.
Akizungumza kabla ya kuridhiwa kwa ajenda hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndg. Tito P. Mganwa amesema mfuko wa elimu ni suala la mkakati wa kitaifa kwa kila Halmashauri kuwa na mfuko wa elimu.
“Suala la uanzishwaji wa mfuko wa elimu lina sura mbili la kwanza ni mkakati wa kitaifa kwa kila Halmashauri iwe na mfuko wa elimu ndio maana kulikuwa na rasimu ya uanzishwaji wa mfuko wa elimu ya mwaka 2010, kulikuwa na rasimu tena iliyokuja kuhuishwa na kusainiwa na Mhe. Jafo mwaka 2021”. Amesema Ndg. Mganwa.
Akiendelea baada ya kuridhiwa kwa ajenda hiyo Ndg. Mganwa amehaidi kusimamia mfuko huo wa elimu ili kufanya kazi kama ulivyokusudiwa.
“Mimi pia kama katibu na Mtendaji Mkuu wa Baraza lenu nawaahidi kwamba tutasimamia na kuhakikisha kuwa mfuko unafanya kazi iliyokusudiwa ili zile changamoto zinazojitokeza kwemye masuala ya elimu ziweze kutatuliwa na mfuko huu”. Alisema Ndg. Mganwa.
Aidha, kupitia mkutano huo wa Baraza la Madiwani Mhe. Edson Sweti Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino amepongeza Idara za Elimu Msingi na Sekondari kwa kufanya vizuri katika matokeo ya mtihani wàTaifa wa kidato cha nne ya mwaka 2024 kwa kushika nafas ya 4 ukilinganisha na matokeo ya mwaka 2023 na kupanda kwa nafasi 4 katika Mkoa wa Dodoma na kwa kushika nafasi ya 3 kàtika mtihani wa Taifa wa darasa la saba.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.