Na Brian Machange - Chamwino
Serikali imetoa wiki mbili kwa wananchi waliovamia eneo la Farm katika kijiji cha Chamwino Ikulu mkoani Dodoma kuondoka katika eneo hilo kuanzia Oktoba 2, 2021 kwa kuwa kijiji hicho kilishatangazwa tangu mwaka1992.
Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Gift Msuya ametoa agizo hilo baada ya uchunguzi wa mgogoro wa eneo hilo katika kikao chake na wananchi wa kijiji cha Chamwino mkoani Dodoma.
"Natoa tamko la serikali kwa niaba ya kamati ya ulinzi ya wilaya na wananchi wa kijiji cha Chamwino naagiza wanaokalia maeneo ndani ya eneo la Farm kuondoka ndani ya wiki mbili na watakaokaidi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao" amesema Msuya.
Sehemu ya eneo la shamba la Farm lenye ukubwa wa ekari 640 lililoanzishwa kati ya mwaka 1971/1972 na Hayati baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere kwa lengo la kuwafunza wanakijiji cha Chamwino ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa maziwa, mbuzi, kondoo, nguruwe na kuku lilivamiwa na kuzua mgogoro kati ya wananchi na serikali.
Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya ya Chamwino, mwananchi yeyote aliyeingia ndani ya eneo hilo ni marufuku kufanya shughuli yoyote kama vile ujenzi, kilimo na serikali kupitia idara ya ardhi itaweka mabango katika eneo hilo kuonesha kuwa eneo hilo ni eneo la umma.
Mkuu wa idara ya ardhi na mali asili Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino akitoa maelezo kuhusiana na umiliki wa ardhi inayovamiwa na wananchi eneo la Farm kijiji cha Chamwino Ikulu.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.