Kutokana na hali ya uwepo wa mvua chache iliyoathiri shughuli za kilimo na upatikanaji wa chakula kwa wingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, leo tarehe 8 Mei, 2025 Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Edson Sweti amesisitiza mahindi yatakayoletwa na Serikali ili kuleta nafuu ya bei ya chakula kwa Wananchi kupelekwa katika kata zote 36.
Msisitizo huo ameutoa kupitia mkutano wa Baraza la Madiwani wa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024-2025 uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Akizungumza wakati anasisitiza jambo hilo ameomba vyakula hivyo vikiletwa vipelekwe katika kata na sio Tarafa ili kuwarahisishia Wananchi wanaotoka mbali na wa hali ya chini kupata kwa urahisi na kuwapunguzia umbali mrefu wa kutembea kufuata vyakula hivyo.
“Tuonaomba vyakula hivyo vikiletwa katika maeneo yetu wasiweke kwenye Tarafa, kuna Mzee anaenda kununua debe moja anatakiwa kutembea kilomita 30 kwenda kuchukua chakula debe moja bodaboda ni shilingi elfu 10 kwa hiyo tutawaumiza”. Alisema Mhe. Sweti
“Tunaomba Serikali iweze kukaa na kufikiria kwa kina sana kuhusu suala la kuleta chakula katika maeneo yetu, itusaidie angalau kwenye kata pale vijiji vitaweza kupunguza safari kutembea masaa matatu mpaka manne hilo naomba nisisitize sana kwa niaba ya Baraza au kama Mwenyekiti wa Halmashauri mahindi haya yakija kwenye kata 36 yaweze kufika ili iweze kuwa rahisi kuwafikia watu wasiojiweza”. Aliendelea kusisitiza Mhe. Sweti.
Aidha, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Chamwino Mhe. George Malima amelipongeza Baraza hilo la Madiwani kwa kuwa la mfano kwa kuwa na umoja na kuendesha mikutano yake kwa weledi.
“Haya yanatokea kwa kuwa kazi zimefanyika na zinaonekana mmeshirikiana na wakuu wa Idara wote mnaimba wimbo mmoja na Waswahili wanasema ndege wafananao huruka kwa pamoja hongereni sana kwa hilo”. Alipongeza Mhe. Malima.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.