Leo Oktoba 27, 2025 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino imetoa mikopo ya Tsh. 133,000,000 kwa vikundi 24 vya wajasiriamali, ambavyo vimejumuisha vikundi 10 vya vijana, vikundi 13 vya wanawake na kikundi 01 cha walemavu, ikiwa ni utoaji wa mkopo wa 10% kwa makundi hayo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Hafla ya utoaji wa mikopo hiyo imefanyika katika ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, na imehudhuriwa na wataalamu mbalimbali kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Benki ya NMB, pamoja na wanachama wa vikundi mbalimbali vya wajasiriamali ambao ni wanufaika wa mkopo huo.

Akizungumza Katika hafla hiyo, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya, Afisa Tawala wa Wilaya ya Chamwino Ndg. Benjamin Cosmas amesisitiza wanufaika wa mikopo hiyo kuielekeza katika shughuli za kiuchumi walizozianisha wakati wa maombi yao, ili iwaletee manufaa.
“Tunapotumia hii mikopo naomba tujikite katika lengo letu la awali, zile shughuli za kiuchumi ambazo tulizianisha wakati wa kuomba mikopo. Isifike mahali mkaelekeza hizi fedha kwenye matumizi mengine kwasababu mtakuwa manajiandaa kushindwa kuendesha mradi, na kushindwa kufanya marejesho kwa wakati."
kadhalika, amesisitiza ushirikiano, na kusikilizana miongoni mwa wanavikundi ili kuwawezesha kuwa na maamuzi ya pamoja ambayo yatawasaidia kufikia malengo yao.

Pamoja na mambo mengine, wanavikundi wamepewa elimu ya fedha na mtaalamu wa Benki ya NMB pamoja na kujengewa uelewa wa kisheria na mtaalamu wa sheria kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kuhusiana na mikopo hiyo, ili iwaletee tija.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.