Kata, shule na walimu waliyofanya vuzuri katika mitihani ya kitaifa 2024 kwa shule za msingi katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino wamepatiwa tuzo ikiwemo fedha taslimu katika hafla fupi ya kuwapongeza kwa jitihada zao za kuongeza ufaulu kwa Wanafunzi.
Hafla hiyo ya kuwapongeza na kuwazawadia ambayo ilibeba kauli mbiu “Chamwino Bila D na E Inawezekana” imefanyika Jumamosi tarehe 10 Mei, 2025 katika ukumbi wa Simba Hotel mbele ya mgeni rasmi Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri na Mdhibiti Ubora wa Shule Wilaya ya Chamwino Ndg. John Balisidya.
Zawadi na fedha hizo zilijumuisha ufaulu katika masomo ya Hisabati, Kingereza, Sayansi, Uraia, Kiswahili, Maarifa ya Jamii pamoja na tuzo kwa wafanyakazi bora ambapo Kata za Buigiri, Msanga na Chamwino ni miongoni mwa Kata zilizoibuka kidedea kwa kuongoza ufaulu.
Akizungumza katika ugawaji wa zawadi hizo Bi. Zaina Kishegwe Afisa Elimu na Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ambao ni waratibu wa hafla na utowaji wa tuzo hizo amewapongeza na kuwaomba walimu kuongeza jitihada ili kuongeza ufaulu na kufuta alama D na E kwa Wanafunzi katika mitihani ya Kitaifa inayofuata.
“Nina uhakika kuwa kwa asilimia 100 kila mmoja akisimama kwa nafasi yake akatekeleza yale ambayo tumekubaliana kuna uwezekano kabisa Chamwino tukafuta kabisa ufaulu wa D na E, na ni naamini Chamwino tukawa na ufaulu wa asilimia 100”. Alisema Bi. Kishegwe.
Aidha, kwa upande wake mgeni rasmi Kaimu Mkurugenzi Ndg. John Balisidya pia amewapongeza walimu hao kwa kufanya vizuri na kuwaomba ambao hawakubahatika kupata tuzo kuhakikisha wanafanya vizuri ili nao waweze kupata tuzo hizo mwaka 2025.
“Kuanzia mwaka 2018 tumekuwa tukienda mjongeo chanya mjongeo huo chanya si unaenda tu peke yake bali kuna watendaji ambao ni nyinyi mnayoifanya kazi hiyo ya kila siku na ni kazi nzito, ngumu lakini hamchoki na hamkati tamaa, hongereni sana”. Alipongeza Ndg. Balisidya.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.