Kamati ya Kudumu ya Bunge la Bajeti imeridhishwa na mwenendo wa utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa Wilayani Chamwino ikiwemo mradi wa Bwawa la Membe na mradi wa Skimu ya umwagiliaji Chinangali chini ya Mradi wa Building Better Tomorrow (BBT)
Akizungumza Leo Novemba 11,2023 Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mbunge wa Kilindi Mkoani Tanga Mhe. Omary Kigua wakati wa ziara ya Kamati hiyo iliyoanzia Mkoa wa Dodoma na inatarajia kufanyika kwa siku saba katika Mikoa mingine tofauti tofauti ikiwemo Manyara, Arusha, Singida, Tabora ,Iringa na kukamilika katika Mkoa wa Mbeya, amesema ziara hiyo ina lengo la kutembelea na kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa na Wizara ya Kilimo.
“Tumeridhika na shughuli zinazoendelea hapa na kiasi cha fedha ambacho kimetumika hakika kinasadifu kwamba kazi mnaisimamia vizuri ". Ameeleza Mhe. Kigua.
Aidha, amewaomba wananchi wa Kata ya Membe kutoa ushirikiano kwa Serikali popote utakapo hitajika kwani mradi huo utakapokamilika utakwenda kuwainua kiuchumi wananchi wote waliopo maeneo jirani na maeneo hayo ya miradi kwa kuwa wao ndio watakuwa wanufaika wa kwanza na hiyo ndiyo dhamira ya Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuinua maisha ya wananchi wa kipato cha chini.
Kwa Upande Wake, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde ametumia fursa hiyo kuelezea azma ya Serikali katika kuhakikisha wanamuwezesha mkulima kuzalisha kipindi chote cha mwaka bila kutegemea mvua.
“ Lengo letu kama Wizara tunataka Wananchi waweze kufanya shughuli za Kilimo mara mbili hadi tatu kwa mwaka wasitegemee mvua , Pia mradi huu hautakua kwa ajili ya kilimo tu bali hata wafugaji watatengenezewa banio kwa ajili ya kunyweshea ng'ombe na shughuli za uvuvi pia zitafanyika.” Amesema Silinde
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule amemshukuru Mhe. Rais kwa kufanya Mapinduzi ya Kilimo ndani ya Mkoa huo ambayo yatasaidia kuondoa njaa ,udumavu na kitakuwa chanzo cha uchumi kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Ameahidi kuendelea kuwa karibu na wakandarasi ili fedha zilizotolewa na Serikali ziweze kufanyiwa kazi husika kama ilivyokusudiwa na kwa ufanisi .
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.