"Fanyeni Kazi Kama Vikundi Pasipo Kutegeana", Mhe. Mayanja
Vikundi vya wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu Wilaya ya Chamwino wametakiwa kufanya kazi kama vikundi pasipo kutegeana kutekeleza majukumu kama walivyokaa na kuandika andiko la mradi na kulipekeka Halmashauri.
Hayo yamesemwa leo April 11, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Janeth Mayanja kwenye hafla ya kukabidhi hundi ya mikopo kwa vikundi hivyo yenye thamani ya Shilingi 144,472,000/=
Akitoa mfano amesema kuna wanakikundi walianzisha mradi wa ufugaji wa kuku lakini wakategeana katika kuwahudumia na mwisho wake kuku wote wakafa.
"Kuna kikundi kimoja nafahamu walikuwa wanafuga kuku mkoa mwingine kabisa, wakawekeana utaratibu wa zamu ya kuwapa kuku dawa, kusafisha banda, kuwapa chakula. Siku moja niliwatembelea nikabaini kwamba kikundi kimewaachia ile kazi kama watu wawili, mtu ikifika zamu yake kila siku anatoa udhuru." Alisema Mhe. Mayanja.
"Walioonyesha ushirikiano walikuwa wawili na baadae wale wawili wakaanza kuambizana kwani hii kazi ni ya kwetu binafsi, wakaanza na wao kutegea mwisho wa siku kuku wakafa, mradi ukafa na deni wakawa wanaendelea kudaiwa." Alisema Mhe. Mayanja
Aliendelea kueleza kuwa leo wamepewa mikopo isiwe watakapofanya ufuatiliaji wakute anayeuelewa mradi ni mtu mmoja au wawili, kwani hata wakishindwa kulipa hatua zitakazochukuliwa ni kwa kikundi chote. Hivyo wote wanapaswa kusimama na kuvuka pamoja na malengo ya kikundi kutimia. Wanavikundi mnapaswa kurejesha mkopo ili kuwa na sifa ya kukopesheka kwa wakati mwingine.
Aidha mkuu wa Wilaya ameeleza kuwa mahitaji ya wanaohitaji mkopo huko vijijini ni makubwa kuliko wanaopata mikopo hiyo. Amewaomba wakawe mabalozi kwa kuwa wamepata fedha kutoka Halmashauri kama kuna mtu atajitokeza kwenye maeneo yao akasema hakuna mikopo wawe wa kwanza kujitokeza kutoa ushuhuda.
Amewaasa wawe na nidhamu ya fedha na muda. Wasiende kubadilisha matumizi ya fedha na kupelekea miradi kukwama na hivyo mikopo hiyo kutoacha alama kwenye maisha yao.
Pia amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mikopo hiyo kutolewa pasipokuwa na riba.
Nao wanavikundi waliopatiwa mkopo wakiwakilishwa na Esaya Jonas, Anna Sospeter na Oscar Ayub kwa nyakati tofauti wamemshukuru Mhe. Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa mikopo hiyo pamoja na Halmashauri na kueleza kuwa mikopo hiyo itawawezesha kujikwamua kiuchumi na kuahidi kurejesha kwa uaminifu ili na wengine waweze kunufaika kama wao.
Naye Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ndugu Godfrey Mnyamale ameelza kuwa fedha za kukopesha bado zipo hivyo wawapelekee habari hizo na vikundi vingine ili watume maombi na baada ya kuhakikiwa na kukidhi vigezo waweze kupatiwa mikopo.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.