Wakazi wa kijiji cha Chinangali II, Mwegamile na kata ya Buigiri kwa ujumla wameaswa kuzingatia masuala ya malezi kwa watoto na kuepuka kufanya masuala ya ukatili. Imeelezwa kuwa katika zama hizi wazazi na walezi wengi wamejisahau katika suala la malezi ya watoto kitu kinachopelekea watoto wengi kufanyiwa vitendo vya ukatili na kuwa na tabia mbaya.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chamwino Kamanda Grace Peter Salia kwenye mkutano wa hadhara uliotishwa na Mhe Diwani wa kata ya Buigiri kwa lengo la kuwahamasisha wazazi na walezi kuchangia chakula shuleni ili wanafunzi waweze kupata chakula wakiwa shuleni, uliofanyika Machi 04, 2025 shule ya msingi Chinangali II.
" kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, wanawake wenzangu tuangalie malezi ya watoto wetu na familia zetu, hata vitabu vya Mungu vinatuelekeza hivyo. Tujue wajibu wetu ni kwenye familia, jamii na Taifa kwa ujumla." Alisema Kamanda Salia.
Aidha kamanda wa Polisi Kata ya Msanga aliendelea kuwasisitiza wazazi juu ya suala la malezi na kueleza kuwa kwa sasa kumekuwa na wimbi kubwa la watoto wa mitaani kutokana na wazazi wengi kupuuzia suala la malezi.
'Mzazi ungetimiza wajibu wako mtoto wako asingekataa shule, anaktaa kwenda shule sababu humuhimizi kwenda shule. Mtoto anakuwa mwizi kwa sababu humfundishi tabia njema. Kwenye alezi wazazi wanachangia mzazi unamtukana mtoto matusi makubwa hapo unategemea nini?" Alisema Kamanda.
Aliendelea kueleza kuwa Mzazi akiona mtoto wake ameharibika anakimbilia kumpeleka polisi wamsaidie kumrekebisha kama wewe mzazi unayeishi naye siku zote amekushinda, Polisi ataweza kumrekebisha kwa muda mfupi?
Vilevile aliwaelekeza wanawake kuwapenda watoto wa kambo na kuacha kuwafanyia ukatili maana hawakujileta duniani.
Kamanda Salia pia alipongeza kwa hatua walizochukua za kukabiliana na uhalifu kwenye eneo lao kwa kushirikisha jamii kwani polisi peke yao hawawezi kuzuia uhalifu huo pasipokushirikiana na jamii kwa sababu wahalifu wanaishi kwenye maeneo yao.
"Anayejua wahalifu ni nyinyi wanajamii, mkiamua kwa wazi na kuwabaini wahalifu na kuleta taarifa Polisi kupitia mikutano yetu ya vijiji na vitongoji, sisi hatutawaangusha. Tutawachukulia hatua za kisheria na mwisho wa siku watafungwa. Alisema Kamanda Salia."
"Lakini watu wengine wanaficha wahalifu, tukiamua kuzuia uhalifu tunaanza kauli mbiu Familia yangu haina uhalifu, kila familia ikiamua ikasema familia yangu haitakuwa na uhalifu maeneo yetu hayatakuwa na uhalifu. Akaja mgeni ambaye haeleweki ukamripoti kwa mwenyekiti wa kitongojikama ni mhalifu atachukuliwa hatua. Hivyo niwaombe kupitia viongozi wenu wa vijiji na vitongoji mtusaidie kutoa taarifa za uharifu zinazotokea kwenye maeneo yenu." Alisema Kamanda Salia.
Aliwaomba waendelee kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi, hivyo kila mtu anawajibu katika ulinzi shirikishi.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.