Wakulima Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino wahamasishwa kuunda vyama vya ushirika ili waweze kuuza mazao yao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa ajili ya kujiongezea kipato.
Wito huo umetolewa leo tarehe 9 Julai, 2025 katika kikao cha Baraza la Biashara la Wilaya ya Chamwino ambacho kiliongozwa na Mwenyekiti na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Janeth Mayanja kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Pia wito huo umetolewa kufuatia manufaa makubwa yaliyoletwa na mfumo wa stakabadhi ghalani katika minada miwili iliyofanyika katika kata ya Dabalo mwezi Juni 2025 ambapo Wakulima wa zao la Ufuta walijipatia takribani shilingi milioni 605, hivyo kuleta chachu ya kuundwa kwa vikundi vya ushirika katika maeneo mengine ili wakulima waweze kunufaika.
Akihimiza kuundwa kwa vyama vya hivyo vya ushirika Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mh. Janeth Mayanja ameitaka Halmashauri kuhamasisha na kuanzisha vyama vya ushirikika hasa maeneo yanayolimwa zao la ufuta ili wakulima waweze kunufaika.
“Halmashauri ianze uhamasishaji na kuanzisha vyama vya ushirika kwenye maeneo unapolimwa ufuta ili msimu unaokuja pia ufuta huo uuzwe kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kama ilivyofanyika hapo Dabalo”. Alihimiza Mh. Mayanja.
Pamoja na hilo Mhe. Mayanja amekemea tabia za baadhi ya Wafanyabiashara kupotosha Wakulima juu ya kutumia mfumo wa stakabdhi ghalani ili kuwapotezea fursa Wakulima ya kujipatia kipato kwa lengo la kunufaisha maslahi yao.
“Hawa Wakulima tuna kazi kubwa ya kuwajengea uwezo huyu mfanyabiashara wa mazao hapa katikati ukimwambia twende kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani hayupo tayari kwasababu yeye alikuwa ananunua shilingi 1000 halafu ufuta hapa unauzwa shilingi 2400 anaona dili kwake limekufa kwahiyo huyu mfanyabiashara ndiye anayeeneza sumu kwa wakulima”. Alikemea Mhe. Mayanja
Sanjari na hilo, ametoa wito pia kwa kutolewa kwa elimu kwa Wananchi kulima mazao yanayostahimili na kuendana na hali ya hewa katika maeneo yao ili kuepusha Wananchi kutumia gharama kupanda mazao ambayo hayatostawi katika maeneo yao.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji Ndg. Tito Mganwa amewahakikishia wafanyabiashara kuwa Halmashauri itaharakisha ujenzi wa machinjio ya mifugo katika Kata ya Chamwino ili Wananchi waweze kupata kitoweo kilichobora na salama kwa matumizi yao.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.