Katika mapambano ya kuongeza ufaulu wa Wanafunzi shuleni ndani ya kata ya Buigiri na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kwa ujumla, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri na Diwani wa kata ya Buigiri Mh. Kenneth E. Yindi ameongoza mkutano na wazazi wa Kijiji cha Mwegamile na Chinangali II Kata ya Buigiri uliofanyika katika shule ya Msingi Chinangali II.
Mkutano huo umefanyika jana tarehe 04 Machi, 2024 ikiwa ni hitimisho la ziara ya Mh. Yindi katika kata ya Buigiri kutembelea shule zote za Msingi na Sekondari na kuzungumza na wazazi kutatua changamoto mbalimbali shuleni ikiwemo upatikanaji wa chakula katika shule zote.
Akizungumza katika mkutano huo amehimiza Wazazi kuchangia chakula shuleni ili Wanafunzi waweze kula muda wa shule
“Kushuka kwa elimu ni kwa kukosa chakula shuleni, hiyo hela unayoitoa itasababisha maendeleo baadae." Alihimiza Mh. Yindi.
Pamoja na hilo, amewasisitiza waalimu kuwa na matumizi mazuri ya michango inayokusanywa shuleni kwa ajili ya chakula.
“Kwenye michango hiyo hiyo zile kamati zilizochaguliwa, Waalimu hizi hela mzione kama moto Wazazi wanahitajika kwa asilimia mia moja na washirikishwe kwenywe kila kitu”. Alisema Mh. Yindi.
Aidha Mhe. Diwani amewaelekeza walimu kufuata sheria ya utoaji wa adhabu za viboko kwa Wanafunzi shuleni kuhaidi kuchukua hatua kwa Waalimu ambao watawaadhibu Wanafunzi maeneo ya mwili yasiyostahili.
Halikadhalika, katika ziara zake hizo katika vijjiji vyote vya kata ya Buigiri, Makamu Mwenyekiti ametoa michango mbalimbali katika shule zote za kata ya Buigiri kuchangia chakula na kutatua changamoto mbalimbali katika kufanikisha upatikanaji wa chakula shuleni ikiwemo kilo 600 za mahindi, kilo 350 za maharage, kilo 175 za mbaazi, kilo 50 za kunde, majiko 10 ya gesi kwa shule zote pamoja na Zahanati ya Mwegamile, zahanati ya Buigiri na Ofisi ya Kata, mabati kwa ajili ya ujenzi wa majiko pamoja na fedha taslimu.
Vilevile Kamanda wa Polisi Wlaya ya Chamwino Grace Peter Salia aliahidi kuchangia kiasi cha shilingi 100,000/= kwa ajili ya kununua mlingoti wa bendera na kamba kwa ajili ya shule ya Sekondari ya Mwengamile ambapo kiasi cha shilingi 20,000/= kilitolewa na Mwenyekiti wa kijiji cha Buigiri kama sehemu ya mchango huo.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.