Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino imepongezwa kwa kuanzisha mfuko wa elimu. Pongezi hizo zimetolewa jana tarehe 18 Februari, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mh. Janeth Mayanja wakati wa kikao cha wadau wa elimu Wilayani Chamwino kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Ikumbukwe Baraza la Madiwani la robo ya pili ya mwaka 2024-2025 lililofanyika tarehe 30 Januari, 2025 liliridhia kwa pamoja kuanzisha mfuko wa elimu kwa nia ya kutatua changamoto na kuongeza ubora wa elimu Halmashauri ya Chamwino.
“Nawapongeza Halmashauri kwa kuchakata mchakato wa kuanzisha mfuko wa elimu wa Halmashauri, wale wote mliohusika kwa namna moja ama nyingine mjipigie makofi”. Alipongeza Mh. Mayanja.
Akiendelea kutoa pongezi hizo Mh. Mayanja ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho aliwapongeza Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkurugenzi Mtendaji na Madiwani kwa kuacha alama kwa kuanzisha mfuko huo.
“Na hizo ndizo alama kwamba wewe Mkurugenzi na Mwenyekiti wakati wa uongozi wenu mliweka alama ya kauanzisha mfuko wa elimu na nyinyi Madiwani wakati wa uwepo wenu mlitengeneza mfuko wa elimu, kwasababu mfuko wa elimu utaenda kuwasomesha hata watoto wanaotoka katika mazingira magumu.” Alisema Mh. Mayanja.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndg. Tito P. Mganwa amesema kutakuwa na mkutano wa uzindizi wa mfuko huo wa elimu na kuanzisha harambee ya kuchangia mfuko huo.
Aidha, kikao hicho cha wadau wa elimu kiliadhimia maadhimio mbalimbali kwa lengo la kuboresha ustawi wa elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.