Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Selemani Jafo amekagua ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino na kuagiza Wakala wa Majengo(TBA) na Suma JKT kuangalia namna bora ya kulifanya jengo hilo liweze kukamilika kwenye ubora unaotakiwa ili watumishi wahamie.
Jafo ametoa agizo hilo wakati wa kukagua utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa mwezi Novemba mwaka jana, ambapo aliagiza ujenzi huo ukamilike ifikapo Januari mosi mwaka huu.
Waziri Jafo amesema pamoja na kuridhishwa na sababu zilizotolewa na Mkandarasi kutokana na kuchelewa kukamilisha ujenzi huo ni vyema wahahakikisha linakuwa na ubora ili liweze kutumiwa na watumishi.
Amebainisha kuwa kwasasa watumishi waendelee kutumia ofisi ya Mkuu wa wilaya hadi hapo litakapokamilika.
Waziri Jafo amewataka kuifanya tathmini hiyo ili wanaelekea katika mipango ya bajeti waangalie namna ya kushirikiana na Halmashauri ili jengo liweze kukamilika.
Awali, Mkandarasi kutoka Suma JKT, Mhandisi David Pallangyo amesema ukamilishaji jengo hilo umekwamishwa kutokana na hali ya hewa kwamba kumekuwepo na uvujaji maji hasa kipindi hichi cha mvua.
“Hapa hii flow ya chini tuliona tuikamilishe lakini hali ya hewa na hizi mvua maji yanajaa hapa juu kwa kuwa hatujaweka paa yanamwagikia chini, tunafanya tathmini kama tutaweza ni vyema tukaweka water proof,” amesema
Aidha Mkandarasi Mshauri kutoka TBA, Mhandisi Vilumba Sanga amesema wanafanya tathmini katika jengo hilo kuangalia namna ya kulikamilisha kwa kushirikiana na Suma JKT.
“Tunafanya ‘estimate’ ya water proof maana maji yanajaa, hii inatokana na makosa yaliyofanywa na mkandarasi wa awali, huyu mkandarasi wa sasa anakutana nayo site,”amesema Sanga
Katika hatua nyingine, Waziri Jafo ametembelea Kituo Cha Afya cha Chamwino Ikulu kuangalia uboreshaji wa kituo hicho ambacho kimeingiziwa Sh.Milioni 500 kwa ajili ya kujenga Wodi ya akina mama na watoto, maabara, Chumba cha Kuhifadhia maiti.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.