Na Mwandishi wetu, Chamwino
SERIKALI, imelegeza masharti ya kukopa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa Halmashauri kwa Vikundi vya Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu ilikuviwezesha vikundi vingi zaidi kukopa.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Nne wa Maafisa Maendeleo Jamii.
Waziri Jafo amesema kuanzia tarehe 26 Februari, 2021 Serikali imerekebisha na kutoa kanuni mpya ambazo zimechapishwa kwenye gazeti la serikali ilizianze kutumika na kuwa moja ya kigezo kilicholegezwa nikupungua kwa idadi ya wanakikundi.
‘Kigezo cha kuwa na idadi ya watu kumi kwa vijana na wanawake na watu watano kwa walemavu, kwa muda mrefu kumechangia kwa baadhi ya watu waliokubaliana na malengo yaliofanana kushindwa kuungana’.
‘Kanuni mpya zinasema kwa vikundi vya vijana na kinamama wakipatikana watano kikundi hicho kinaweza kukopesheka lakini tumeenda mbali zaidi kubadilisha kanuni kumwezesha hata mtu mmoja mwenye ulemavu anaweza kupewa mkopo, haya ni mapinduzi makubwa’ amesema Waziri Jafo.
Amesema kuanza kutumika kwa kanuni hizi mpya kutatoa fursa kwa vikundi vingi kuwa na sifa ya kupata mikopo hiyo.
Waziri Jafo amesema kuwa katika eneo lingine ambalo limeimarishwa ni suala la urahisishwaji wa ufuatiliaji wa mikopo kwa serikali kutenga fungu kulingana na ukopeshaji wa kila mamlaka.
‘Kuanzia sasa kanuni mpya zinaelekeza kwa kila Halmashauri kutenga kiasi cha fedha ili kuwawezesha Maafisa Maendeleo Jamii kufanya tathimini na ufuatiliaji wa mikopo iliyotolewa’
Akifafanua zaidi, Waziri Jafo amesema kwa Halmashauri ambazo mapato yake ya ndani hayazidi shilingi Bilioni moja katika kila marejesho Idara ya Maendeleo ya Jamii itatengewa shilingi laki tano wakati Halmashauri ambazo mapato yake ni zaidi ya shilingi bilioni moja zimeelelezwa kutenga kati ya milioni moja na shilingi milioni moja na nusu kwa mwezi kwa ajili ya ufuatiliaji.
Aidha kwa Halmashauri ambazo mapato yake yapo kati ya shilingi bilioni tano na kuendelea amesema Idara ya Maendeleo ya Jamii ipatiwe shilingi milioni tano kwa ajili ya tathimini na ufuatiliaji.
Sambamba na maboresho hayo, Waziri Jafo ameziagiza mamlaka za serikali za mitaa, kuhakikisha wanawahusisha wataalamu wa maendeleo ya jamii kwenye miradi yote inayotekelezwa katika eneo husika kuanzia hatua za awali.
Amesema kutokana na umuhimu wa Maafisa Maendeleo Jamii kama wahamasishaji wa jamii kwenye shughuli za maendeleo, ameziagiza Mamlaka za Serikali za mitaa kuwashirikisha wataalamu wa kada hii katika miradi yote inayotekelezwa.
Kufuatia kauli hiyo ya Waziri Jafo, akizungumza kwa niaba ya Maafisa Maendeleo Jamii wenzake, Rais mpya wa Chama hicho Angela Kiama, amesema wamepokea kwa furaha mabadiliko ambayo serikali imeifanya katika kanuni.
‘Tatizo lilikuwepo mathalani kwa walemavu, unaweza kukuta mlemavu mmoja katika eneo anashindwa kupewa mkopo kwa kigezo cha kuwataka wawe kikundi, kwakweli tunaishukuru serikali kwa kuliona hili nakufanya maboresho kwenye kanuni hizo’ amesema Kiama.
Maafisa Maendeleo Jamii hao waliokutana kwa siku tatu kutathimini hali ya utendaji kazi sambamba nakuwachagua viongozi wa Chama chao.
Mkutano Mkuu wa Maafisa Maendeleo Jamii, ni wanne tangu kuanzishwa kwa Chama hicho mwaka 2017, na ulikuwa na kauli mbiu ‘Maafisa Maendeleo ya Jamii Nguzo Muhimu kufikia Uchumi wa Viwanda’ na umewashirikisha maafisa wa kada hiyo kutoka serikallini na taasisi binafsi.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.