Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, leo Februari 11, 2026 imetoa mikopo ya shilingi 188,500,000 kwa vikundi 22 vya wajasiriamali vilivyokidhi kupata mikopo hiyo, ambapo shilingi 130,000,000 zimekopeshwa kwa vikundi 17 vya wanawake, na shilingi 58,500,000 kwa vikundi 5 vya vijana.
Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Mhe. Janeth Mayanja ameasa vikundi hivyo kufanya matumizi sahihi ya mikopo hiyo ikiwa ni pamoja na kuelekeza fedha katika miradi inayotekelezeka kama iliyobainishwa wakati wa mchakato wa maombi.
Amesema kwamba, ni muhimu vikundi kujikita katika kuendeleza miradi viliyokwisha anza kutekeleza badala ya kuchepusha mikopo hiyo Kwenda kwenye miradi mipya, kwani uzoefu unaonyesha kwamba kufanya hivyo huwa hakuleti tija inayokusudiwa.
Aidha, ameasa kudumisha ushirikiano na uwazi ili kuwa na maelewano, kwani nyenzo muhimu katika kudumisha mshikamano na kufikia mafanikio ya pamoja, ikiwa ni pamoja na kuwezesha vikundi kufanya marejesho kama ambavyo mkataba wa mkopo unavitaka.
“Mafanikio ya mikopo hii yanategemeana sana na inavyopokelewa, inavyotumika na namna inavyorejeshwa, ni muhimu kuhakikisha kwamba mkopaji ana mradi halisi unaotekelezeka na wenye tija.”
Vikundi vilivyopata mikopo leo vinatoka katika kata za Zajilwa, Membe, Chamwino, Manchali, Msamalo, Igandu, Mvumi misheni, Makang’wa, Loje, Mpwayungu, Huzi na chiboli.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.