Halmashauri ya Wilaya Chamwino terehe 6 Machi, 2025 imeadhimisha siku ya Wanawake Duniani yakiongozwa na mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Janeth Mayanja yaliyofanyika katika viwanja vya Mpwayungu.
Sherehe hizo za maadhimisho hayo yaliyobeba kauli mbiu “Wanawake na Wasichana 2025 Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji” zilitawaliwa na furaha na shamra shamra mbalimbali pamoja na ujumbe uliobebwa kutoka kwa viongozi na wadau waliohudhuria sherehe hizo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Janeth Mayanja amewahasa Wanafunzi wa kike kutoa taarifa kwa mamlaka husika endapo wanakwamishwa kutimiza ndoto zao za masomo na familia zao.
“Watoto wa kike wote waliopo hapa wajue wakipitia changamoto yeyote wakatoe taarifa kwa wenyeviti wa vitongoji, vijiji, watendaji wa vijiji, kata, kwa waheshimiwa madiwani mkatoe taarifa Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha ndoto zenu zinatimia”. Alisema Mh. Mayanja.
Akiendelea na suala la elimu kwa mtoto wa kike amewahasa wazazi kuwaachia watoto wao urithi wa elimu.
“Na katika hili niwaombe Wazazi na Walezi na Wananchi wote waliokusanyika mahali hapa hakuna urithi pekee ambao tunaweza tukawapa watoto wetu isipokuwa elimu unaweza kumpa nyumba ikatokea tetemeko nyumba ikabomoka, lakini mtoto wako akipata elimu ni urithi wake wa milele”. Alisema Mh. Mayanja.
Aidha, zawadi mbalimbali na vyeti vya pongezi zilitolewa kwa Wanawake ambao wameonesha juhudi za kujituma na kushiriki uhamasishaji wa masuala mtambuka katika jamii.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.